Jun 14, 2021 02:29 UTC
  • Wananchi wa Morocco wakataa majengo yao yageuzwe ubalozi wa Israel

Wamiliki wa majengo na majumba katika mji mkuu wa Morocco, Rabat wamekataa kata kata kukodisha majengo yao kwa ajili ya kutumika kama ofisi za uwakilishi za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Televisheni ya al-Jazeera imenukuu vyombo vya habari vya Morocco na vya Kizayuni vikiripoti kuwa, David Govrin, mwakilishi wa Israel nchini Morocco angali anafanyia kazi hotelini, miezi sita baada ya kuwasili katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Inaarifiwa kuwa, maafisa wa wakala uliopewa jukumu la kutafuta jengo la kuweka ofisi za kibalozi za Israel mjini Rabat wanaelekea kusalimu amri, kwani kila mmliki wa jengo anapojua litatumika kama ofisi za uwakilishi wa utawala pandikizi wa Israel hukataa kata kata kulikodisha.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, Govrin ambaye amewahi kuwa balozi wa utawala haramu wa Israel nchini Misri amejifungia hotelini tangu alipowasili nchini Morocco Januari mwaka huu.

Haya yanajiri huku maelfu ya watu wa Morocco wawakiendeleza kampeni katika mitandao ya kijamii ya kutaka mwakilishi huyo wa utawala wa Kizayuni wa Israel nchini humo atimuliwe mara moja.

Wamorocco katika maandamano ya kuilaani Israel na kuwaunga mkono Wapalestina

Disemba mwaka jana Morocco na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel zilisaini mapatano ya kuanzisha uhusiano baina yao na kisha Marekani ikatambua rasmi mamlaka ya udhibiti wa Morocco kwa eneo la Sahara Magharibi. 

Morocco ni nchi ya sita ya Kiarabu baada ya Jordan, Misri, Imarati, Bahrain na Sudan  kuanzisha uhusiano kati yake na utawala ghasibu wa Kizayuni.  Kitendo hicho cha Morocco cha kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel ambacho ni sawa na kusaliti malengo ya Palestina kimekabiliwa na radiamali hasi katika Ulimwengu wa Kiislamu na hata ndani ya Morocco kwenyewe.

Tags