Jun 14, 2021 02:32 UTC
  • Baada ya US kuondoa askari wake Somalia, sasa yawatuma Kenya

Rais wa Marekani, Joe Biden ametangaza kuwa serikali yake itatuma vikosi maalumu vya wanajeshi nchini Kenya, eti kwenda kusaidia juhudi za kupambana na magaidi wa kundi la ukufurishaji la al-Shabaab.

Kupitia barua kwa Bunge la Congress, Rais Biden amesema ameidhinisha kutumwa kwa vikosi maalumu nchini Kenya, ambavyo vinatarajiwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo (KDF) kupambana na wanamgambo wa al-Shabaab.

Barua hiyo ya Biden kwa Congress ya Marekani hata hivyo haikutaja idadi ya askari watakaotumwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki. 

Ikumbukwe kuwa, mtangulizi wa Biden, Donald Trump mwaka uliopita kabla ya kuondoka ofisini alitoa amri ya kuondolewa nchini Somalia kwa askari wanaokadiriwa kuwa 700 wa Marekani kufikia Januari 15 mwaka huu.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilisema wakati huo kwamba, wanajeshi hao watatumwa katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki, pengine Kenya au Djibouti; eti kuendeleza vita dhidi ya ugaidi.

Askari vamizi wa US nchini Somalia 

Askari hao wa Marekani wamekuwepo nchini Somalia kwa kisingizio cha kuvisaidia vikosi vya serikali ya Mogadishu katika operesheni zake za kukabiliana na wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab. Kenya yenyewe ina maelfu ya askari wanaofanya kazi chini Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom).

Viongozi wa mataifa ya Afrika daima wamekuwa wakitaka majeshi vamizi ya Marekani yaondoke katika nchi zao, wakisisitiza kuwa, kuendelea kuwepo askari wa nchi hiyo ya kibeberu katika nchi zao hakuna matokeo mengine ghairi ya kuzidi kuvuruga amani na usalama sambamba na kuenea harakati za makundi ya kigaidi.

Tags