Jun 14, 2021 08:11 UTC
  • Algeria yaifungia kanali ya Ufaransa ya

Serikali ya Algeria imeipokonya kanali ya televisheni ya Ufaransa ya France 24 leseni ya kuhudumu nchini humo, siku moja baada ya kufanyika uchaguzi wa Bunge katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Msemaji wa Serikali na pia Wizara ya Habari ya Algeria, Ammar Belhimer amesema "hatua ya kuifungia kanali hiyo ya habari ya satalaiti imetokana na kitendo chake cha kukariri wazi wazi uhasama dhidi ya taifa letu na taasisi zake."

Serikali ya Algiers ilikuwa imeipa France 24 onyo la mwisho mnamo Machi 13, na kuitaka iwache kurusha habari za kiuhasama, kichochezi na kuichafua serikali ya nchi hiyo.

Ufaransa haijatoa taarifa kuhusu uamuzi huo, lakini usimamizi wa kanali hiyo ya dola umedai kuwa umeshangazwa na hatua ya kufungiwa kwa sababu tu ya eti kurusha matangazo yao kwa uwazi, uhuru na ukweli.

Algeria na mkoloni wake huyo wa zamani wa Ulaya zimekuwa zikivutana na kulumbana kwa miaka mingi sasa juu ya mambo mbali mbali.

Ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria

Hivi karibuni, Waziri wa Kazi wa Algeria alitoa taarifa rasmi na huku akiashiria ripoti zilizofichua kwamba Ufaransa ilifanya majaribio ya nyuklia katika ardhi ya Algeria alisema, "mkoloni huyo wa Ulaya ataendelea daima na milele kuwa adui wa taifa letu, kama ambavyo hivi sasa pia Ufaransa ni adui mkongwe na wa zamani sana wa Algeria."

El Hachemi Djaaboub alisema hayo na kuongeza kuwa, jeshi la Algeria limeitaka Ufaransa iwalipe fidia wananchi wa Algeria kutokana na kufanya majaribio ya nyuklia katika ardhi ya nchi hiyo miaka 60 iliyopita na kuhatarisha usalama wa wananchi wa Algeria tangu wakati huo hadi hivi sasa.

Tags