Jun 14, 2021 13:04 UTC
  • Ripoti: Kuna aina 30 za virusi vya COVID-19 Afrika Kusini

Wataalamu wa afya wa Afrika Kusini wameeleza kuwa kuna uwezekano kwamba nchi hiyo ina zaidi ya aina 30 za virusi vya COVID-19 vilivyobadilika.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa katika tovuti ya Independent Online, wataalamu Afrika Kusini wana wasiwasi kuwa, wagonjwa wa UKIMWI wa hali mbaya wanaweza kuwa “Viwanda vya COVID-19 vinavyobadilika”. 

Mwezi Septemba mwaka 2020, baada ya mwanamke mwenye virusi vya Ukimwi mkoani Kwazulu-Natal kugunduliwa kuwa na COVID-19, wanasayansi wa Afrika Kusini waligundua kuwa virusi hivyo vilitengeneza protini Spike protein 13 vilivyobadilika na mabadiliko mengine 13 ya jeni yatakayoweza kubadilisha virusi.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 36 amekuwa na virusi vya Corona kwa siku 216 na katika kioindi hicho virusi hivyo vilibadilika mara 30.

 Hadi sasa wanasayansi bado hawajui kama mwanamke huyo ameambukiza wengine virusi hivyo vilivyobadilika. Wanasayansi wameeleza kuwa bado utafiti unahitajika zaidi kujua kama watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuambukizwa virusi vya Corona na kutengeneza aina mpya za virusi.

Hayo yanajiri wakati ambao hivi karibuni, Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa Afrika (Africa CDC) kilitangaza kuwa, hadi sasa nchi za Afrika zimepata dozi milioni 55 za chanjo za COVID-19. Kwa mujibu wa taarifa, ni asilimia 0.6 ya watu wa bara la Afrika pekee ndio waliopata chanjo kamili ya COVID-19 hadi kufikia Alhamisi ya jana.

Kati ya nchi za Afrika, nchi tano zilizopata dozi nyingi zaidi za chanjo hizo ni Morocco, Misri, Nigeria, Ethiopia na Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa takwimu za Africa CDC, hadi sasa vipimo zaidi ya milioni 49 vya virusi vya Corona vimefanywa na nchi za Afrika, na kiwango cha jumla cha matokeo chanya au walioambukizwa ni asilimia 10.1.