Jun 15, 2021 07:42 UTC
  • UN yawawekea vikwazo vinara wa kundi la kigaidi la Al Shabab

Vinara watatu wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab wameingizwa katika orodha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa ili kusaidia serikali ya Somalia kupambana na kundi hilo.

Akizungumza Jumatatu katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Geraldine Byrne Nason Balozi wa Kudumu wa Ireland katika umoja huo ambaye pia  ni Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Azimio nambari 751 (1992) kuhusu Somalia amesema waliowekewa vikwazo wanashikilia nyadhifa muhimu katika kundi hilo la kigaidi.

Nason alieleza wasiwasi wake juu ya ripoti za ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu na kubainisha kuwa taratibu madhubuti za kudhibiti silaha na risasi za serikali ya Somalia ni muhimu katika kuzuia kundi la Al-Shabab na kundi jingine linalofungamana na ISIS kupata vifaa vya kijeshi.

Kundi la kigaidi la al-Shabab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Umoja wa Mataifa unafadhili askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo (AMISOM) ambao sasa ni 21,000 na wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 kwa lengo la kukabiliana na magaidi hao wa Al Shabab.

Tags