Jun 16, 2021 02:35 UTC
  • Makurutu 15 wa kijeshi wauawa katika shambulio la kigaidi, Somalia

Kwa akali makurutu 15 wameuawa katika shambulio linaloaminika kuwa la kigaidi katika kambi moja ya mafunzo ya kijeshi huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Afisa wa Jeshi la Somalia, Mohamed Adan amesema gaidi aliyejiripua katika shambulio hilo la 'kujitoa muhanga' alijipenyeza katika Kambi ya Kijeshi ya Jenerali Dhegobadan akijifanya mmoja wa makurutu na kisha kutekeleza hujuma hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, majeruhi wa shambulio hilo la jana Jumanne wamepelekwa katika Hospitali ya Madina mjini Mogadishu.

Hadi tunamaliza kuandaa habari hii, hakuna kundi lililokuwa limetangaza kufanya hujuma hiyo, ingawaje kundi la kigaidi la al-Shabaab na magenge yenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda yamekuwa yakihusika na mshambulio ya namna hii. 

Mmoja wa majeruhi akiwahishwa kwenye ambulensi

Kundi la kigaidi la al-Shaabab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Umoja wa Mataifa unafadhili askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo (AMISOM) ambao sasa ni 21,000 na wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 kwa lengo la kukabiliana na magaidi hao wakufurishaji.

Tags