Jun 16, 2021 12:24 UTC
  • Kenya yatuma wanajeshi wake DRC kujiunga na MONUSCO

Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) limetuma askari wake wa Kikosi cha Radiamali ya Haraka huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwenda kusaidia jitihada za kupambana na magenge ya kigaidi na makundi yanayobeba silaha.

Mkuu wa Majeshi ya Kenya, Jenerali Robert Kibochi alikikabidhi kikosi hicho bendera ya nchi hiyo jana Jumanne katika kambi ya jeshi ya Embakassi jijini Nairobi, ishara ya kukibariki kiondoke nchini na kwenda kujiunga na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo DR (MONUSCO). Kikosi cha MONUSCO kwa sasa kinaundwa na wanajeshi wa Tanzania, Afrika Kusini na Nepal.

Jenerali Kibochi amekiasa kikosi hicho kudumisha nidhamu ya hali ya juu na kutii miongozo yote ya maadili ya Umoja wa Mataifa. Kikosi hicho kitakita kambi katika eneo la Mavivi, mjini Beni mashariki mwa Kongo DR.

Kenya imetuma wanajeshi wake wa kulinda amani DRC siku chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuitembelea nchi hiyo na kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Felix Tshisekedi.

Wanajeshi wa MONUSCO mashariki mwa DRC

Ongezeko la mashambulizi ya magenge yenye silaha na machafuko ya kikabila yamesababisha vifo vya mamia ya watu tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, huku wanajeshi wa serikali na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakijaribu kuleta utulivu mashariki mwa nchi hiyo bila mafanikio.

Kundi la ADF ambalo asili yake ni Uganda na ambalo linasemekana kuwa na mfungamano na genge la kigaidi la ISIS (Daesh) limeua raia zaidi ya 1,000 tokea Novemba mwaka 2019 katika mji wa Beni pekee, mashariki mwa Kongo DR.

Tags