Jun 17, 2021 02:27 UTC
  • Ethiopia yapinga azimio la Arab League kuhusu Bwawa la Renaissance

Ethiopia imepinga na kukosoa vikali azimio lililopasishwa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu linalolitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liingilie kati mgogoro juu ya Bwawa la al-Nahdha.

Katika taarifa, Addis Ababa imesema imesikitishwa na hatua ya Misri na Sudan ya kujaribu kuingiza siasa pasi na udharura wowote katika mgogoro huo.

Taarifa ya serikali ya Ethiopia imesema ni jambo la kusikitisha kuziona Cairo na Khartoum zinafanya juu chini kuyageuza mazungumzo ya mgogoro wa bwawa hilo kuwa kadhia ya Kiarabu.

Jana Jumanne, Arab League ilitoa taarifa ya mwisho baada ya mkutano wake na kusema kuwa, Baraza la Usalama la UN linapaswa kuchukua hatua za makusudi na kuzindua 'mchakato wa mazungumzo amilifu' yatakayolenga kufikiwa makubaliano ndani ya muda maalumu utakaoainishwa.

Mkutano wa Arab League

Hivi karibuni, Kamanda wa Jeshi la Anga la Ethiopia alitangaza kuwa, jeshi hilo lipo tayari kulilinda bwawa hilo na kukabiliana na uchokozi wa aina yoyote.

Hii ni katika hali ambayo, nchi hiyo ikiwa imedhamiria kuanza awamu ya pili ya kujaza maji katika Bwawa la Reinassance mwezi ujao japokuwa Misri, Sudan na nchi hiyo bado hazijafikia mapatano kuhusu suala hilo.  

Tags