Jun 17, 2021 02:29 UTC
  • Mamia ya wakimbizi wa Kongo DR wamiminika Uganda

Wakimbizi karibu elfu moja raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamewasili nchini Uganda katika kipindi cha siku chache zilizopita.

Irene Nakasiita, Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda amesema wakimbizi wapatao 950 wamewasili katika wilaya ya Bundibugyo, iliyoko magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Ghasia, machafuko na mapigano huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamepelekea raia hao wa DRC ama kufurushwa kutoka makwao au kulazimika kukimbilia usalama wao nchini Uganda katika kipindi cha siku chache zilizopita.

Afisa huyo wa Msalaba Mwekundu nchini Uganda amesema miongoni mwa wakimbizi Wakongomani waliowasili nchini humo, 664 ni watoto wadogo, 175 wanawake na wanaume 135.

Wakimbizi Wakongomani nchini Uganda

Amesema wasiwasi mkubwa walionao ni kushindwa kuwafuatilia baadhi ya wakimbizi hao, ambao wanaishia kutangamana na jamaa zao wanaoishi nchini Uganda. 

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR zinaonesha kuwa, Uganda ni mwenyeji wa wakimbizi wapatao milioni moja na laki nne, aghalabu wakitokea DRC, Sudan Kusini na Rwanda.

 

Tags