Jun 17, 2021 12:32 UTC
  • Nigeria: Kifo cha kiongozi wa Boko Haram kimethibitishwa bila shaka yoyote

Kifo cha aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la wanamgambo wa Boko Haram wenye makao yao nchini Nigeria kimethibitishwa pasina shaka yoyote. Taarifa hiyo imetolewa kupitia tangazo kwa njia ya video lililotolewa na kiongozi mpya wa Boko Haram, Bakura Modu.

Kuthibitishwa kifo cha Abubakar Shekau kumehitimisha mlolongo wa tetesi zilizokuwa zikiendelea tangu mwezi Mei mwaka huu kuhusu hatima ya gaidi huyo. 

Weledi wa mambo wanasema kuwa, Bakura Modu aliyeteuliwa kuwa kiongozi mpya wa genge la kigaidi la Boko Haram anaishi katika eneo la Lake Chad. Kiongozi huyo mpya wa Boko Haram amemtuhumu Abu Musabb al Barnawi kiongozi wa kundi la wanamgambo la ISWAP lililojitenga na Boko Haram kuwa ndiye aliyemuuwa Abubakar Shekau. 

Abubakar Shekau enzi za uhai wake na magaidi wenzake wa Boko Haram 

Katika ujumbe wake alioutuma kwa lugha ya Kiarabu Bakura Modu ametoa wito kwa kulipiza kisasi dhidi ya kundi hasimu la ISWAP ambalo liliasisiwa mwaka 2016 baada ya kujitenga na Boko Haram.

Abubakar Shekau ambaye alichukua uongozi baada ya kufa Mohammed Yusuf kiongozi mwingine wa Boko Haram mwaka 2009 anadaiwa kujilipua kufuatia mzozo uliokuwa ukiendelea kati ya Boko Haram na hasimu wake yaani kundi la wanamgambo wa ISWAP katika msitu wa Sambisa huko kaskazini mashariki mwa Nigeria. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Sheria ya Marekani, Abubakar bin Mohammad al Shekau alizaliwa kati ya mwaka 1965 na 1975. Wazazi wake walitokea kusini mwa Nigeria. Alikulia katika kijiji cha Yobe kaskazini mwa Nigeria kabla ya kuelekea Maiduguri katika jimbo la Borno ambako alijikita katika misimamo ya kufurutu ada na kujiunga na Boko Haram. 

Tags