Jun 18, 2021 02:26 UTC
  • Sudan yavunjwa moyo na matokeo ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel

Miezi kadhaa baada ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel kama njia ya kujikurubisha kwa Marekani na kupata misaada ya kifedha ya nchi hiyo, serikali ya Sudan imeeleza kuvunjwa moyo na matokeo ya hatua hiyo baada ya kunyimwa misaada hiyo.

Maafisa wa serikali ya Khartoum wametangaza kuwa, Marekani haikutekeleza ahadi yake ya kuwekeza katika miradi ya kilimo na teknolojia nchini Sudan na kusisitiza kuwa, wamevunjwa moyo na matokeo ya hatua ya nchi hiyo ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sudan ilikuwa nchi ya tatu ya Kiarabu baada ya Imarati na Bahrain ambazo zilisaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel, na tarehe 6 Januari mwaka huu ilisaini makubaliano hayo rasmi kwa mashinikizo ya aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump. Maafisa wa Sudan walikuwa na matumaini kwamba, kutia saini makubaliano hayo kungeiwezesha nchi hiyo kupewa misaada ya kifedha na kisiasa ya Washington, mtetezi mkubwa zaidi wa utawala wa Kizayuni, na kwamba madeni yake yangesamehewa au kulipwa na waitifaki wa Marekani. Mkabala wa hatua hiyo ya kukubali kuanzisha uhusiano na Israel pia, Sudan iliomba msaada wa chakula wenye thamani ya dola bilioni 1.2, msaada wa fedha taslimu dola bilioni 2 au mkopo wa miaka 25. 

Watu wa Sudan wakichoma bendera ya Israel

Hivi sasa baada ya kupita karibu miezi 8 tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Sudan na utawala haramu wa Israel na safari za mara kwa mara za viongozi wa Tel Aviv kwenda Sudan na kinyume chake, na vilevile mahusiano na Wasudani na Wamarekani, Washington haijatimiza ahadi zake kwa Khartoum. Si hayo tu, bali miezi kadhaa iliyopita Sudan ililipa fidia kwa Marekani kwa shabaha ya kutolewa jina la nchi hiyo katika orodha nyeusi ya Washington eti ya makundi ya kigaidi. Kuhusu suala hilo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken anasema: Washington imepokea dola milioni 335 kutoka Sudan kama fidia ya wahanga wa mashambulizi ya mabomu yaliyolenga balozi za nchi hiyo katika miji ya Dar es Salaam huko Tanzania na Nairobi nchini Kenya mwaka 1999, shambulizi lililolenga manowari ya USS Cole mwaka 2000 na vilevile mauaji ya mwanadiplomasia wa Marekani John Granville aliyeuawa kwa kupigwa risasi mjini Khartoum tarehe Mosi Januari mwaka 2008.

Hata hivyo licha ya kujikomba kote huko Sudan haijapewa himaya au misaada ya kifedha ya Marekani na waitifaki wake, na viongozi wa sasa wa serikali ya Khartoum wamekuwa wakisema kuwa, hawajafaidika na muamala huo, na badala yake matatizo ya kiuchumi na kisiasa na nchi hiyo yanaongezeka kila uchao. Miezi michache zilizopita Waziri wa Habari wa Sudan, Faisal Muhammad Saleh alisema kwamba, yaliyozungumzwa kuhusu kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na kwamba sera hiyo itaziletea amani na utulivu pande zilizofanya mapatano hayo ni njozi tupu.

Wasudani wakikabiliana na askari usalama

Hali ya kisiasa na kiuchumi ya Sudan inaendelea kudorora na kuporomoka na vyama vya upinzani vinaendelea kupaza sauti vikipinga hatua ya serikali ya Khartoum ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel. Wasudani wengi wanasumbuliwa na mgogoro wa chakula na kushindwa kukidhi mahitaji yao ya kila siku kutokana na hali ngumu ya maisha, na mfumuko wa bei za bidhaa muhimu umefikia asilimia 350. Uhaba wa maji na kukatika umeme mara kwa mara vinashuhudiwa katika miji mikubwa ya Sudan na kuibua maandamano ya wananchi wanaozidiwa na hali ngumu ya maisha. Kwa madiri kwamba, juzi Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok aliyekuwa akihutubia taifa alitahadharisha kuhusu hatari ya kutokea machafuko na vita vya ndani.

Kutokana na hali hiyo, Sayyid Qassem Zakery ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: Sudan inaelekea kuwa kituo kipya cha machafuko na ukosefu wa amani kwenye eneo la Pembe ya Afrika; kwa msingi huo wafuatiliaji wa mambo wanasema yumkini nchi hiyo ikakumbwa na hatima kama ile ya Somalia na Yemen.         

Tags