Jun 18, 2021 07:10 UTC
  • WHO: Virusi vya corona vinasambaa kwa kasi kubwa barani Afrika

Ofisi ya Shirika la Afya Dunia (WHO) barani Afrika imetangaza kuwa, wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya corona linatapakaa kwa kasi kubwa katika nchi za bara la Afrika.

Mkurugenzi wa WHO barani Afrika ameeleza wasiwasi wake kuhusu wimbi la tatu la maambukizi ya aina mbalimbali za virusi vya corona barani humo na kusema kuwa, idadi ya watu wanaoambukizwa virusi hivyo kila wiki barani Afrika imeongezeka kwa aslimia 22. 

Taarifa ya WHO imesema kuwa, kwa sasa watu milioni 12 katika nchi za Afrika wamepata chanjo kamili ya virusi vya corona lakini imetahadharisha kuwa kiwango hicho ni sawa na chini ya asilimia moja ya jamii ya watu wa Afrika.

Shirika la Afya Duniani limesema kwa sasa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Uganda ndizo zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya kila siku ya corona. Limesema kirusi hatari cha corona aina ya Delta kimezikumba nchi 14 za Afrika na aina za Beta na Alpha zimeshuhudiwa katika nchi 25 za bara hilo.

Takwimu zinaonesha kuwa nchi za Afrika Kusini, Moroco, Tunisia, Ethiopia, Misri na Libya ndio zenye idadi kubwa zaidi ya waathiriwa wa virusi vya corona. Afrika Kusini na Misri ndizo zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu walioaga dunia kutokana na virusi hivyo barani Afrika.