Jun 21, 2021 02:53 UTC
  • Nchi za Magharibi mwa Afrika kuzindua sarafu moja mwaka 2027

Jumuiya ya Uchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS imepasisha ramani mpya ya njia ya uzinduzi wa sarafu moja mwaka 2027, baada ya mpango wa awali wa kuzindua sarafu hiyo kuvurugwa na janga la Corona.

Rais wa Kamisheni ya ECOWAS, Jean-Claude Kassi Brou amewaambia waandishi wa habari baada ya kufanyika Kongamano la Viongozi wa jumuiya hiyo katika mji mkuu wa Ghana, Accra kwamba, viongozi wote wa nchi wanachama wameafikia suala la kufanya uzinduzi huo mwaka 2027.

Nchi wanachama wa ECOWAS zinatarajia kuwa, matumizi ya sarafu hiyo iliyopewa jina la 'Eco' yatapiga jeki biashara na ustawi wa chumi za nchi hizo za Magharibi mwa Afrika.

Rais wa Kamisheni ya Jumuiya ya Uchumi ya Magharibi mwa Afrika amebainisha kuwa, ramani hiyo ya njia kuelekea uzinduzi wa sarafu ya Eco itaanza kutekelezwa mwaka ujao 2022 hadi 2026, na kisha mwaka utaofuata (2027) ndio uzinduzi rasmi wa sarafu yenyewe utakapofanyika.

Sarafu ya ECO itakayotumiwa na nchi za ECOWAS

Baada ya uzinduzi huo, nchi hizo zitaanza kufanya miamala yao ya kibiashara kwa kutumia sarafu hiyo ya pamoja ya Eco ili kuepukana na madhara na hasara ya mabadilishano ya kifedha yanayosababishwa na kutumia sarafu ya Faranga ya Ufaransa.

Ukiondoa Guinea Bissau, nchi saba zingine zote zilizoamua kujitoa kwenye utumiaji wa sarafu ya Faranga, ambazo ni Ivory Coast, Burkina Faso, Benin, Mali, Senegal, Niger na Togo zilikuwa makoloni ya zamani ya Ufaransa.

Tags