Jun 21, 2021 06:51 UTC
  • Magaidi 15 wa al Shabab waangamizwa nchini Somalia

Jeshi la Somalia limetangaza habari ya kuangamizwa wanachama 15 wa genge la kigaidi na ukufurishaji la al Shabab nchini humo.

Jeshi la Somalia limetangaza hayo usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa, askari wa nchi hiyo wamefanikiwa kuzima shambulio la genge la kigaidi la al Shabab katika kambi moja ya kijeshi kwenye eneo la Diinsoor na kuangamiza magaidi 15 wa genge hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya jeshi la Somalia, askari wa nchi hiyo wamechukua ngawira zana zote za kijeshi za magaidi hao na sasa hivi wanaendelea kuwasaka magaidi wengine waliokimbia.

Siku chache zilizopita pia, wanafunzi 15 waliuawa katika shambulio la kigaidi kwenye kambi moja ya mafunzo ya kijeshi huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Wanajeshi wa Somalia

 

Afisa wa Jeshi la Somalia, Mohamed Adan alisema kuwa, gaidi aliyejiripua katika shambulio hilo la alijipenyeza katika Kambi ya Kijeshi ya Jenerali Dhegobadan akijifanya mmoja wa makuruta na kisha kujiripua.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, majeruhi wa shambulio hilo la Jumanne iliyopita walipelekwa katika Hospitali ya Madina mjini Mogadishu.

Mara kwa mara jeshi la Somalia hulipiza kisasi mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na genge la ukufurishaji la al Shabab.

Hivi karibuni pia, Mohamed Abdullahi, kamanda wa Kikosi cha 60 cha Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) alisema kuwa, wanachama 12 wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab wameangamizwa kwenye operesheni ya jeshi la Somalia katika eneo la Bay la kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.