Jun 21, 2021 12:42 UTC
  • Wasichana wahajiri wa Kiafrika wananajisiwa na hata kupewa ujauzito katika kambi ya EU, Libya

Kundi la wasichana wahamiaji waliowekwa katika kituo kinachosimamiwa na serikali ya Libya wamewashutumu walinzi wa kituo hicho, kinachofadhiliwa na Umoja wa Ulaya, kwamba wanawabaka na kuwanyanyasa kingono.

Msichana wa Kisomali mwenye umri wa miaka 17 ambaye utambulisho wake haukutajwa kwa sababu za kiusalama, ameliambia shirika la habari la AP kwamba alibakwa na mlinzi katika kituo cha Shara al-Zawiya katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, mwezi Aprili mwaka huu.

Wasichana zaidi wamejitokeza katika kituo hicho na kutoa madai kama hayo ya kubakwa na kunajisiwa na walinzi na askari usalama wa Libya katika kituo hicho kilichoanzishwa na Umoja wa Ulaya.

Wasichana hao waliokolewa na vikosi vya usalama vya Libya mwezi Februari zaidi ya miaka miwili iliopita baada ya kukamatwa na wafanyabiashara ya magendo ya binadamu, ambao waliwadhalilisha vibaya kingono. Wafanyamagendo hao wanajulikana kwa kuwatesa na kuwanyanyasa wahamiaji na wakimbizi wanaopitia Libya wakijaribu kuelekea Ulaya.

Msichana huyo wa Kisomali mwenye umri wa miaka 17 amesema aliendelea kubakwa na kunajisiwa hata kwenye kituo kinachosimamiwa na serikali ambako wahamiaji wengi au wakimbizi wanahifadhiwa.

"Ingawa sio mara ya kwanza kupata mateso kama haya ya kunajisiwa, lakini unyanyasaji wa mara hii ni mchungu zaidi kwa sababu unafanywa na watu ambao wanapaswa kutulinda," amesisitiza msichana huyo mwenye umri wa miaka 17.

Amesema: "Lazima utoe kitu kwa ajili ya kuruhusiwa kwenda bafuni, kupigia simu familia au kuepuka kupigwa,  kana kwamba tunashikiliwa na wafanyamagendo ya binadamu."

Wahajiri wa Kiafrika Libya

Tarik Lamloum ambaye ni mwanaharakati anayefanya kazi na Shirika la Haki za Binadamu la Belaady nchini Libya amethibitisha kuwa: "Ukatili na unyanyasaji wa kingono umeshamiri sana katika vituo kadhaa vya wafungwa na wahamiaji kote nchini."

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa pia limethibitisha kuwa mamia ya wanawake wamebakwa wakiwa katika kambi za Idara ya Kupambana na Uhamiaji Haramu zinazosimamiwa na serikali ya Libya, (DCIM) au magereza ya wafanyamagendo ya binadamu, na kwamba wasichana wengine wamepewa ujauzito na walinzi na kujifungua wakiwa mahabusu. 

Tags