Jun 22, 2021 10:57 UTC
  • Kura za uchaguzi wa Bunge Ethiopia zaendelea kuhesabiwa, mahudhurio ya wananchi yalikuwa makubwa

Mchakato wa kuhesabu kura za uchaguzi wa Bunge na serikali za mitaa unaendelea nchini Ethiopia huku yombo vya usalama vikisema umefanyika kwa amani na usalama, ukitupilia mbali malalamiko machache ya hapa na pale.

Vyombo vya habari vinaripoti kwamba uchaguzi huo umeshirikisha idadi kubwa ya watu kuliko ilivyotabiriwa hapo awali licha ya kususiwa na vyama vikuu vya upinzani. 

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uchaguzi ya Ethiopia, Birtukan Mideksa amesema kuwa, zoezi la kuhesabu kura limeanza kote nchini na matokeo yake yatatangazwa baada ya kuthibitishwa na kupasishwa na vyombo husika. Amesema matokeo kamili ya uchaguzi muhimu wa Bunge la Ethiopia yatatangazwa katika kipindi cha siku kumi zijazo.

Kamisheni ya Uchaguzi ya Ethiopia ililazimika kurefusha muda wa kupiga kura kote nchini humo kwa masaa mtatu zaidi kutokana na safu ndefe zilizokuwa kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kumalizika muda uliokuwa umetangazwa hapo awali.

Waethiopia milioni 37 walikuwa wametimiza masharti ya kupiga kura kwa ajili ya kuchagua wabunge 547 kati ya wagombea wote zaidi ya elfu nane wa vyama 46 vya siasa waliojiandikisha kuwania viti hivyo. Idadi ya waliojisajili kupiga kura imetajwa kuwa ni ndogo ikizingatiwa kuwa Ethiopia ina jamii ya watu milioni 110.

Upigaji kura uliahirishwa katika maeneo bunge 110 kati ya jumla ya 547, kwa sababu ya vurugu na matatizo ya vifaa vya kupigia kura, na haukufanyika katika mikoa ya Tigray (Kaskazini) na Somalia (Ogaden) mashariki mwa Ethiopiai.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema uchaguzi huo ni ushahidi kwamba anashikamana na kuheshimu demokrasia. Ameongeza kuwa, uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki, na kwamba ndio utakaokuwa wa kidemokrasia zaidi katika historia ya Ethiopia.

Tags