Jun 22, 2021 10:58 UTC
  • Awamu ya kwanza ya kuzalisha chanjo ya corona kuanza Afrika Kusini

Afrika Kusini itakuwa mwenyeji wa kituo cha kwanza cha uzalishaji wa chanjo ya Covid-19 barani Afrika.

Kwa msaada wa Shirika la Afya Duniani (WHO), maafisa wa Afrika Kusini wanapanga kuanzisha kituo cha uhamishaji wa teknolojia ya chanjo ya Covid 19 ambacho kitakuwa cha kwanza cha aina yake barani Afrika.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuhusiana na suala hilo kwamba, kituo hicho cha kuhamisha teknolojia kitatumika kwa ajili ya kutoa mafunzo ambako watengenezaji wa chanjo kutoka nchi zenye kipato cha chini au kati watapata mafunzo kuhusu uzlishaji wa baadhi ya chanjo na kupata ruhusa na kuzalisha chanjo hiyo.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa lengo la mpango huo ni kuwa na uwezo bora zaidi wa kusambaza chanjo ya corona katika bara la Afrika. Ramaphosa ameongeza kuwa, sasa Afrika imeelewa kwamba dozi za corona kamwe hazitakuja kutoka mahali pengine kwa wakati ili kuokoa maisha ya Waafrika.

Cyril Ramaphosa

Ramaphosa ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba "Uwezo wa kutengeneza chanjo, dawa na bidhaa zingine zinazohusiana na afya utasaidia kuiweka Afrika katika njia ya kujitegemea."

"Imedhihirika wazi kwamba, hatuwezi kuendelea kutegemea chanjo ambazo zimetengenezwa nje ya Afrika, kwa sababu haziletwi Afrika; na zikiletwa hazifiki kwa wakati mwafaka, na watu wanaendelea kufariki dunia", amesisitiza Rais wa Afrika Kusini. 

Afrika Kusini inaongoza kwa kuwa na asilimia 35 ya waathirika wote wa virusi vya corona barani Afrika.