Jun 23, 2021 07:16 UTC
  • Mariam al-Sadiq al-Mahdi
    Mariam al-Sadiq al-Mahdi

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Sudan ametoa wito wa kuitishwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kujadili mgogo wa ujenzi wa Bwawa la Renaissance juu ya maji ya Mto Nile nchini Ethiopia.

Mariam al-Sadiq al-Mahdi ameliandikia barua rasmi Baraza la Usalama la UN akiomba kuitishwa kikao cha kuchunguza hitilafu zilizopo baina ya nchi hiyo, Misri na Ethiopia juu ya ujenzi wa  Bwawa la Renaissance na athari zake mbaya kwa maisha na usalama  wa mamilioni ya wakazi wa kandokando ya Mto Nile katika nchi za Misri na Sudan.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Sudan, Omar al Faroq Sayyid Kamal amesema, katika barua yake Waziri wa Mambo ya Nje amemuomba Mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Usalama azitake pande zote kuheshimu ahadi na majukumu yao na kujiepusha na hatua yoyote ya upande mmoja na vilevile aitake Ethiopia isitishe kujaza maji kikamilifu katika  Bwawa la Renaissance. 

Ujenzi wa bwawa hilo juu ya maji ya Mto Nile umezusha mivutano baina ya Ethiopia na nchi za Sudan na Misri.

Bwawa la Renaissance

Misri na Sudan zinasema ujenzi wa bwawa hilo ambalo umegharimu karibu dola bilioni nne, utapunguza maji ya nchi hizo na hivyo kuvuruga maisha ya mamilioni ya watu. Ethiopia nayo inasisitiza kuwa ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kwa ajili ya kueneza umeme katika nchi hiyo ili kuimarisha sekta ya viwanda na pia kuuza bidhaa hiyo katika nchi za nje. Mzozo huo umezusha wasiwasi wa kutokea vita na mapigano baina ya nchi hizo tatu.

Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema kuwa ujenzi wa Bwawa la Renaissance utakuwa na faida si kwa nchi hiyo pekee bali pia kwa nchi za Misri na Sudan.