Jun 23, 2021 13:15 UTC
  • UN: Sudan Kusini bado haina amani kamili

Sudan Kusini inaenda kutimiza muongo mmoja tangu kupata uhuru wake lakini Umoja wa Mataifa unasema bado kuna kazi kubwa ya kufanywa kwani baadhi ya makubaliano hayatekelezwi, watu wenye nia mbaya wanaendelea kuwatesa raia na wafanyakazi wa mashirika ya misaada nao wanavamiwa na kuuawa.

Nicholas Haysom Mwakilishi mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini katika taarifa yake kwa Baraza la Usalama anasema misaada ya kimataifa imesalia kuwa kitu muhimu wakati huu wanajitahidi kupata amani, usalama na ustawi kwa raia wake lakini mwendo ni wa kinyonga.

Amesema utekelezaji wa makubaliano yaliyofufuliwa kwa ujumla unaenda polepole na uundaji wa Bunge bado haujakamilika. Aidha  amesema Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS inaendelea kuihamasisha serikali ikamilishe michakato huku tukihakikisha kuna uwakilishi wa kutosha wa wanawake na vijana.

Magari ya Umoja wa Mataifa Sudan Kusini

Haysom pia amezungumzia hali ya usalama ambayo imekuwa ikisuasua baada ya watu wenye silaha kuwavamia wanavijiji na kufanya uharibifu, katika kipindi cha mwaka huu wa 2021 na asilimia 80 ya walioumia ni wanajamii lakini kubwa linalomtia shaka ni mauaji ya watumishi wa mashirika ya kimataifa na uporaji wa misaada ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Sudan Kusini inakabiliwa na uhaba wa chakula pamoja na utapiamlo ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wake hawana uhakika wa chakula.