Jun 23, 2021 13:19 UTC
  • Wanaharakati Afrika walaani nchi tajiri kuhodhi chanjo za COVID-19

Wanaharakati barani Afrika wanasema, hatua ya nchi tajiri kuhodhi chanjo ya COVID-19 kinakwamisha maendeleo ya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo barani Afrika.

Mkurugenzi wa Mfuko wa Huduma ya Afya ya UKIMWI (AHF) nchini Kenya Samuel Kinyanjui amesema, kuhodhi chanjo kunaongeza uhaba wa kitu kinachoweza kuokoa maisha barani Afrika, ambako maambukizi mapya yanayoongezeka yanatishia mifumo ya afya ya umma barani humo.

Ametoa wito kwa nchi tajiri kusambaza chanjo zinazozidi mahitaji yao, kuondoa hakimiliki na kuunga mkono kuanzishwa kwa viwanda vya kutengeneza chanjo hiyo barani Afrika.

Naye mwenyekiti wa kikanda wa Mtandao wa Taifa wa Watu Waishio na UKIMWI nchini Zimbabwe Moreni Masanzu amesema, utaifa wa chanjo ni kikwazo kikubwa katika juhudi za Afrika kupambana na janga hilo.

Ameongeza kuwa upatikanaji wa chanjo ulio na usawa utanufaisha nchi tajiri na maskini, kwani inaweza kuzuia mabadiliko ya virusi vyenye uwezo mkubwa wa kuambukiza na kurudisha hali ya kawaida katika maisha yetu haraka iwezekanavyo.

Hivi karibuni Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa Afrika (Africa CDC) kilitangaza kuwa, hadi sasa nchi za Afrika zimepata dozi milioni 55 za chanjo za COVID-19.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na shirika la habari la Xinhua, ni asilimia 0.6 ya watu wa bara la Afrika pekee ndio waliopata chanjo kamili ya COVID-19 hadi kufikia Alhamisi ya jana.

Kati ya nchi za Afrika, nchi tano zilizopata dozi nyingi zaidi za chanjo hizo ni Morocco, Misri, Nigeria, Ethiopia na Afrika Kusini.