Jun 23, 2021 13:23 UTC
  • Magaidi waua maafisa 11 wa polisi Burkina Faso

Maafisa 11 wa polisi wameuawa na wengine wanne hawajulikani walipo nchini Burkina Faso katika hujuma inayoaminika kutekelezwa na magaidi wakufurishaji.

Maafisa hao wameuawa wakati walipokuwa wakijitayarisha kuchukua nafasi za wenzao waliokuwa kwenye doria kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa tarifa ya wizara ya usalama, shambulio hilo lilitokea Jumatatu Juni 22 majira ya saa tisa mchana.

Kwa mujibu wa mashuhuda walionusurika katika tukio hilo, washambuliaji walizingira magari na ndipo wakatumia silaha aina ya roketi dhidi ya msafara wa magari ya polisi, ambapo kutokana na silaha duni, polisi hao walilazimika kurudi nyuma.

Maafisa wa usalama Burkina Faso

Hivi karibuni Jeshi la Burkina Faso lilitangaza kuwa magaidi 25 wameuliwa katika oparesheni iliyofanywa na askari wa jeshi hilo.

Burkina Faso nchi inayopatikana katika eneo la Sahel barani Afrika imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya wanamgambo wenye misimamo mikali na magaidi wakufurishaji kwa muda wa miaka sita sasa.