Jun 30, 2021 02:27 UTC
  • Uganda yaidhinisha matumizi ya dawa ya asili 'kutibu Corona'

Serikali ya Uganda imeidhinisha matumizi ya dawa ya mitishamba ya 'Covidex' kwa ajili ya kutibu magonjwa yanayosababishwa na virusi ukiwemo ugonjwa wa Covid-19.

Katika kikao na waandishi wa habari jana Jumanne mjini Kampala, David Nahamya, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Dawa (NDA) amesema baada ya kufanya uchunguzi wa kina, sasa taasisi hiyo ya serikali imeidhinisha rasmi matumizi ya Covidex kwa ajili ya kusaidia kupambana na magonjwa ambukizi yanayotokana na virusi.

Awali, mamlaka hiyo ilikuwa imepiga marufuku matumizi ya dawa hiyo ya asili iliyozalishwa na timu ya wanasayansi wa nchi hiyo wakiongozwa na Profesa Patrick Ogwang wa Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia cha Mbarara.

Hata hivyo licha ya marufuku hiyo lakini wananchi wa Uganda waliendelea kuinunua dawa hiyo kwa wingi pamoja na bei yake kuongezeka maradufu.

Nahamya amesisitiza kuwa, dawa hiyo ya mitishamba haitibu Corona moja kwa moja, lakini inaweza kutumiwa pamoja na dawa zingine wanazopewa wagonjwa wa Covid-19.

Kampeni ya chanjo ya Corona Uganda

Hali ya maambukizo ya Corona nchini Uganda si nzuri kiasi kwamba, baada ya wimbi jipya la maambukizi ya Covid-19 kuivamia Uganda na ambalo limekuja kwa kasi kubwa na hatari zaidi, mamlaka za afya za nchi hiyo zimewataka wafanyakazi wake wavae barakoa mbili mbili ili kupunguza maambukizo ya ugonjwa huo ambao ni janga la dunia nzima.

Aidha shule zote nchini humo zimefungwa kama njia moja ya kudhibiti msambao wa virusi hivyo. Hadi kufikia jana Jumanne, nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilikuwa imesajili kesi zaidi ya 79 elfu za watu walioambukizwa maradhi hayo, huku karibu elfu moja miongoni mwa wakiaga dunia.

Tags