Jul 04, 2021 13:34 UTC
  • Rais wa Uganda ataka kuimarisha uhusiano wa nchi yake na serikali mpya ya Iran

Rais wa Uganda amemtumia ujumbe Rais mteule wa Iran, Sayyid Ebrahim Raeisi akimpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; huku akieleza kuwa Kampala ipo tayari kuimarisha uhusiano wake na serikali ijayo ya Tehran.

Rais Yoweri Museveni amempongeza Hujjatul Islam Walmuslimin Ebrahim Raeisi kwa niaba yake binafsi na kwa niaba ya taifa hilo la Afrika Mashariki, kwa kuibuka mshindi katika Uchaguzi wa Rais wa Juni 18 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kampala, Museveni katika ujumbe wake huo wa tahania amesema Uganda inajivunia kuwa na uhusiano mzuri na Iran, na kueleza matumaini yake kuwa uhusiano huo wa pande mbili utaimarika zaidi katika uongozi wa Raeisi.

Wakati huo huo, Rais Joko Widodo wa Indonesia amemtumia pia ujumbe wa pongezi Ayatullah Sayyid Ebrahim Raeisi kwa kupata ushindi katika Uchaguzi wa Rais wa mwezi uliopita hapa nchini Iran.

Widodo amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni katika washirika muhimu wa nchi hiyo katika eneo, na kwamba uhusiano wa nchi mbili hizi za Kiislamu una umri wa zaidi ya miaka 70.

Wairani wakisherehekea ushindi wa Raisi katika uchaguzi wa Juni 18

Rais Widodo amesema Indonesia imejitolea kwa dhati kuendeleza na hata kunyanyua katika kiwango cha juu zaidi ushirikiano wa pande mbili ambao mbali na kulinda maslahi ya nchi mbili hizi, lakini pia una mchango mkubwa katika kulinda amani ya kieneo na kimataifa.

Sayyid Ebrahem Raeisi aliibuka mshindi katika kinyang'anyiro hicho cha urais cha Juni 18 mwaka huu, kwa kupata kura karibu milioni 18 za wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu.

Tags