Jul 15, 2021 12:36 UTC

Serikali ya Rwanda imetangaza marufuku ya kutoka nje kwa muda wa siku 10 katika mji mkuu, Kigali na wilaya nane baada ya kuripotiwa ongezeko la idadi ya vifo na wagonjwa wa COVID-19 nchini humo.

Watu wametakiwa kutotoka nje ya nyumba zao kuanzia Jumamosi tarehe 17 mpaka tarehe 26 Julai ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Rwanda imechukua uamuzi huo katika mkutano wa baraza la mawaziri mapema jana chini ya Rais Paul Kagame. 

Biashara, usafiri na shughuli za umma, shule, michezo na burudani vyote vimefungwa, na watu 15 tu ndio wanaoruhusiwa kuhudhuria shuhuli zamazishi. Watu wanaruhusiwa kutoka nje ya nyumba zao kwa ajili ya kupata huduma muhimu kama matibabu n.k.

 

Mji mkuu Kigali katika siku 10 za lockdown 

Maofisa wa afya wamesema kusambaa kwa wimbi la tatu la kirusi kipya cha Delta kumeifanya Rwanda ikabiliwe na hali mbaya. Rwanda ambayo hadi kufikia jana jioni ilikuwa imesajili kesi za maambukizi ya Covid-19 zipatazo elfu 50 na 742 na vifo 607 imesema kuwa kesi mpya za maambukizi ya corona zimeongezeka mara nne tangu mwezi Juni mwaka huu; huku idadi ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini pia ikiongezeka pakubwa. Ongezeko kubwa la maambukizi ya corona nchini Rwanda limetajwa kusababishwa na  wananchi kupuuza na kutofuata kikamilifu miongozo na protokali za afya.  

Licha ya zuio hilo la kutotoka nje, shughuli za utalii zitaendelea kama kawaida kwa kufuata protokali za afya ili kuzuia maambukizi ya corona. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali pia utaendelea kuwa wazi huku wasafiri wanaowasili nchini wakitakiwa kuonyesha cheti cha kipimo cha Covid-19 kilichochukuliwa katika kipindi kisichozidi masaa 72. 

Nchi za Kiafrika zinakabiliwa na wimbi la tatu la virusi vya corona, na visa zaidi ya milioni 6 vimethibitishwa barani humo hadi Jumatano ya jana, huku watu zaidi ya 153,000 wakiripotiwa kuaga dunia kitokana na virusi hivyo.

Tags