Jul 21, 2021 07:53 UTC
  • Wataalamu wathibitisha raia zaidi ya 800 wa Uganda 'wamedungwa' maji wakiambiwa ni chanjo ya Covid-19

Mamlaka za serikali ya Uganda zimesema, watu zaidi 800 na idadi kadhaa ya wateja wa makampuni tofauti katika eneo la jiji la Kampala wamedungwa chanjo bandia ya Covid-19.

 Mamlaka hizo zimeeleza hayo katika ripoti iliyotolewa kufuatia matokeo ya vipimo zilizofanyiwa sampuli kadhaa za chanjo.

Daktari Warren Naamara, mkurugenzi wa kitengo cha uangalizi wa afya katika Ikulu ya Rais amevieleza vyombo vya habari kuwa, watuhumiwa wanaofuatiliwa katika uhalifu huo wa kuwatapeli watu kadhaa na makampuni ni pamoja na daktari ambaye hadi sasa bado hajapatikana.

Naamara amesema, watu hao walipigwa chanjo hizo bandia katika kipindi cha kuanzia Mei 15 hadi Juni 17.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo wa kitengo cha uangalizi wa afya katika Ikulu ya Rais wa Uganda, idadi kadhaa ya zilizoshukiwa kuwa chanjo bandia za Covid-19, zikichanganywa na nyengine halisi zilitumwa maabara ya uhakiki ya Kurugenzi ya Serikali iliyoko Wandegeya na kwa Mamlaka ya Taifa ya Dawa ya nchi hiyo (NDA), kwa ajili ya uhakiki kabla ya kusafirishwa na kupelekwa India ili kufanyiwa ulinganishaji na chanjo halisi za Covid-19.

Taasisi ya Serum ya India iliyotengeneza chanjo za corona zilizotumwa nchini Uganda ilithibitisha kuwa chanjo hizo zilizotiliwa shaka hazikusafirishwa na taasisi hiyo kutumwa nchini humo.

Dokta Naamara amebainisha kuwa, kutokana na uhakiki wa mada zilizomo ndani yake, chanjo hizo bandia zilikuwa zimejazwa maji zaidi ya kitu kingine chochote kile.

Hata hivyo amesema, watu waliopigwa chanjo hizo bandia hawajatiwa miilini mwao kitu chochote chenye sumu au kuhatarishwa maisha yao.

Hadi sasa makachero wa Ikulu ya rais wa Uganda wameshawatia mbaroni wauguzi wawili kutoka Nakawa, Kampala wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo.

Wawili hao wamewekwa mahabusu katika jela ya Kitalya.../

Tags