Jul 22, 2021 10:51 UTC
  • Sudan yaionya Ethiopia kuhusu Bwawa la al Nahdha

Waziri Mkuu wa Sudan ametoa onyo kwa serikali ya Ethioia isichukue uamuzi wowote wa upande mmoja kuhusu mgogoro wa Bwawa la al Nahdha.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Abdalla Hamdok ametoa onyo hilo ili kuizui Ethiopia isichukue hatua yoyote ya upande mmoja kuhusu bwawa hilo. Amesema, Sudan inaendelea kupigania kufikiwa makubaliano yaliyo lazima kutekelezwa na pande zote kuhusiana na Bwawa la al Nahdha.

Waziri Mkuu wa Sudan ameongeza kuwa, nchi yake haitoacha kufanya kila juhudi inayowezekana ili kuhakikisha kunafikiwa makubaliano ya kiuadilifu ya kuzinufaisha nchi zote tatu za Sudan, Ethiopia na Misri.

Abdalla Hamdok

 

Itakumbukwa kuwa, katikati ya mwezi huu wa Julai, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisema baada ya kupata ushindi chama chake katika uchaguzi wa Bunge kwamba, kabla ya bwawa la al Nahdha kuwa na manufaa ya uzalishaji wa nishati, lina manufaa makubwa zaidi kwa Ethiopia katika kutangaza nguvu na mshikamano wa wananchi wake na kwamba serikali yake haitozungumza na yeyote kuhusu manufaa ya kitaifa ya bwawa hilo.

Siku chache zilizopita pia na licha ya kuweko maonyo na vitisho vikali vya Sudan na Misri, lakini duru moja ya masuala ya umwagiliaji maji nchini Ethiopia ilisema kuwa, zoezi la kumimina maji kwa awamu ya pili katika Bwawa la al Nahdha limekamilika.

Kumalizika awamu ya pili ya kumimina maji katika Bwawa la al Nahdha nchini Ethiopia kulitangazwa katika hali ambayo, wabunge wa Misri wamelalamikia kuhusika utawala wa Kizayuni wa Israel katika mzozo wa bwawa hilo baina ya Ethiopia, Misri na Sudan.

Tags