Jul 23, 2021 12:37 UTC
  • Marekani yajitosa sakata la Mbowe, Tanzania yajibu

Kamati Ndogo ya Mambo ya Nje ya Afrika ya Baraza la Wawakilishi la Marekani imeiomba Serikali ya Tanzania imuache huru Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo Chadema, Freeman Mbowe, anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi.

Mbowe anatuhumiwa na Polisi kupanga njama za mauaji ya viongozi wa serikali pamoja na ugaidi.

Wito huo ulitolewa jana Alkhamisi na mwenyekiti wa kamati hiyo Karen Bass, saa kadhaa baada ya jeshi la Polisi Tanzania kutoa taarifa ya kumshikilia Mbowe, kwa ajili ya mahojiano kuhusu tuhuma zinazomkabili.

Katika taarifa yake, Karen amevitaka vyombo vya dola kumwachia huru Mbowe akiwa salama mwenye afya njema.

Freeman Mbowe, pamoja na wanachama wengine 11 wa Chadema walikamatwa na jeshi la Polisi Julai 21 saa 8 usiku wakiwa katika Hoteli ya Kingdom, jijini Mwanza.

Walikamatwa saa chache kabla hawajafanya kongamano la kudai katiba mpya. Hata hivyo kongamano hilo halikufanyika baada ya kujikuta wakiishia mikononi mwa dola.

Kwa mujibu wa jeshi la Poli Mwanza, baada ya Mbowe kuhojiwa kwa tuhuma hizo, alisafirishwa hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kufuatia tuhuma zinazomkabili.

Karen Bass

Akizungumzia tukio hiko, Karen ametoa wito kwa mamlaka za Tanzania kuacha kuwakamata wanasiasa wa upinzani.

Amesema, mara baada ya kuingia madarakani Rais Samia Suluhu Hassan, walikuwa na matumaini kwamba ataibadili hali ya nchi.

"Mamlaka za Tanzania, lazima zimalize ukandamizaji unaozidi kuongezeka wa vyama vya upinzani na viongozi. Kuwakamata watu kinyume cha sheria na kuwaweka kizuizini kunaonyesha upuuzwaji wa sheria, haki za binadamu na haki ya kujieleza na kushirikiana," amesema afisa huyo wa Marekani.

Hata hivyo Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Gerson Msigwa amesema kuhusu matamko hayo kuwa, kila nchi ina taratibu zake na kuongezea kwa kusema "tuliache jeshi la polisi lifanye kazi yake, likimaliza litatueleza".

Msigwa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo amesema, matamko hayo hayawezi kuzuia uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili mtu yeyote, huku akiwataka wananchi kuwa watulivu wakati suala hilo likiendelea kufanyiwa kazi.../

 

 

Tags