Jul 24, 2021 04:35 UTC
  • Watu 29 wameaga dunia kwa Corona nchini Tanzania; maambukizo yaongezeka

Waziri wa Afya wa Tanzania, Dk Dorothy Gwajima amesema hadi sasa jumla ya watu 29 wamefariki dunia kutokana na wimbi la tatu la Covid-19 na kwamba siku ya Alkhamisi pekee kulikuwa na wagonjwa wapya 176.

Idadi hiyo ya kufikia Alkhamisi iliyopita inaifanya Tanzania kuwa na jumla ya wagonjwa 858 wa Covid-19.

Waziri wa Afya wa Tanzania pia amewalaumu baadhi ya viongozi wa Serikali ambao amesema hawashiriki kwenye vita vya kupambana na ugonjwa huo. Amesema hali ya maambukizi ya corona nchini Tanzania siyo nzuri na kwamba serikali itawachukulia hatua viongozi wanaofanya mzaha na ugonjwa huo.

Wakati huo huo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC imetangaza kuwa imezidiwa na idadi ya wagonjwa wa corona wanaohitaji hewa ya Oksijeni ukilinganisha na mitungi 400 inayozalishwa kwa siku huku mgonjwa mmoja akitumia mitungi 8 hadi 10 kwa siku.

Hayo yalisemwa jana Ijumaa na Mkurugenzi Mtendaji Hospitali hiyo, Profesa Gilleard Masenga.

Profesa Masenga amesema kwa siku inatumika mitungi ya Oksijeni zaidi 400 ukilinganisha na uzalishaji wake kwa siku ambayo ina uwezo wa kuzalisha mitungi 400.

Maambukizi ya corona yanaongezeka nchini Tanzania

Profesa Masenga amesema: Kwa siku mgonjwa mmoja anatumia mitungi 8 hadi 10 na kwamba hilo ni tatizo ni kubwa. Vilevile amewataka Watanzania wasifanye mzaha na ugonjwa huo ambao amesema ni hatari sana.

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa corona na kufuata maelekezo yote yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Afya.

Tags