Jul 25, 2021 07:30 UTC
  • Watu waghadhibika mno Uganda baada ya wabunge kupatiwa yuro milioni 25 kununulia magari mapya

Wananchi wa Uganda wameghadhibishwa mno na hatua ya serikali ya kuwapatia wabunge kitita cha yuro milioni 25 kununulia magari mapya ya kifakhari katika nchi hiyo masikini ambayo hivi sasa inahiliki kutokana na janga la dunia nzima la ugonjwa wa Covid-19.

Wakati kesi za maambukizi ya virusi vya corona zinaendelea kuongezeka, serikali imempatia kila mmoja kati ya wabunge wote 529 wa bunge la nchi hiyo shilingi milioni 200, ambazo ni sawa na yuro 48,000 za kununulia gari mpya.

Mnamo tarehe 18 Juni, Rais Yoweri Museveni alitangaza karantini na marufuku nyingine mpya kwa muda usiopungua wiki sita ikiwa ni pamoja na watu kutotembea na kufungwa maskuli, makanisa na mabaa.

Wabunge wamepatiwa fedha hizo, wakati mfanyakazi wa kibarua nchini Uganda analipwa mshahara wa wastani wa shilingi laki moja za nchi hiyo, ambazo ni sawa na yuro 24, huku mshahara wa mwalimu ukiwa ni takriban shilingi 260,000, sawa na yuro 64.

Anet Nana Namata, mtetezi wa haki za binadamu na mkurugenzi mtendaji wa Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu Uganda amesema, haikubaliki serikali kukinunulia magari ya kifakhari kikundi kidogo cha watu bungeni, ambao wanaendelea kupokea mishahara zaidi ya shilingi milioni 30, sawa na dola elfu nane za Marekani, wakati sehemu kubwa ya raia wa nchi hiyo hawawezi kujikimu kwa chakula.

Raia wengi wa Uganda ni masikini

Hatua kama hiyo ambayo ilichukuliwa na serikali mwaka 2018, iliwasha moto wa malalamiko na upinzani wa wananchi walioamua kuvamia bunge kabla ya kutawanywa na vikosi vya usalama.

Uganda, yenye watu milioni 45, imesharekodi kesi 91,710 za maambukizi ya virusi vya corona na vifo vya watu 2,496.

Hii ni katika hali ambayo, ni watu wapatao milioni moja tu ambao wamepatiwa chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 hadi sasa.../

Tags