Jul 26, 2021 12:27 UTC
  • Anayedaiwa kujaribu kumuua Rais wa Mali afia korokoroni

Mshukiwa anayedaiwa kujaribu kumuua Rais wa mpito wa Mali Assimi Goïta kwa kumchoma kisu katika mji mkuu Bamako siku chache zilizopita, ameaga dunia akiwa mikononi mwa vyombo vya usalama.

Mtu huyo ambaye jina lake halijatajwa, alikamatwa na kuwekwa kizuizini na maafisa usalama wa nchi hiyo, akiandamwa na tuhuma za kujaribu kumuua kiongozi huyo wa Mali.

Taarifa iliyotolewa jana Jumapili na serikali ya mpito ya Mali inasema kuwa, "wakati uchunguzi ukiendelea, hali yake (mshukiwa) iliendelea kuwa mbaya na akalazwa hospitalini, lakini kwa bahati mbaya ameaga dunia."

Vyanzo vya habari vimeliambia shirika la habari la AFP kuwa, mshukiwa huo hakuwasilishwa kwa vyombo vya mahakama na kwamba wakuu wa mashitaka tayari walikuwa wamefungua faili la mtuhumiwa huyo anayesemekana kwamba alikuwa mwalimu.

Mkasa huo ulitokea Jumanne iliyopita katika Msikiti Mkuu wa Bamako nchini Mali baada ya ibada ya Swala ya Eidul al-Haj. Mashuhuda wanasema kuwa, tukio hilo lilitokea wakati wa kuanza kutekeleza sunna ya kuchinja.

Ramani ya Mali

Hata hivyo washambuliaji wawili hawakuweza kumdhuru Rais huyo wa muda wa Mali baada ya kudhibitiwa na kukamatwa na walinzi wa Rais kabla ya kumfikia kiongozi huyo.

Kanali Assimi Goita aliongoza mapinduzi ya mwezi Agosti mwaka jana (2020), wakati yeye na maafisa wengine wa jeshi walipomuondoa madarakani Rais aliyechaguliwa Ibrahim Boubacar Keita baada ya maandamano ya wiki kadhaa juu ya ufisadi na mzozo wa muda mrefu wa magaidi wakufurishaji. Mei mwaka huu Rais huyo wa mpito wa Mali aliongoza mapinduzi ya pili na kisha kuunda serikali akiwateua mawaziri wapya ambapo wanajeshi wamepata nyadhifa muhimu.

Tags