Jul 26, 2021 12:28 UTC
  • Waislamu wa Nigeria waadhimisha kumbukizi ya mauaji ya Siku ya Quds

Wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) wameadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya makumi ya wanachama wenzao waliouawa na wanajeshi wa Nigeria mwaka 2014, wakati wa maandamano ya kulaani ukatili wanaofanyiwa Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel, wakati wa Siku ya Kimataifa ya Quds.

Wakati wa kongamano la maadhimisho hayo yaliyofanyika jana Jumapili mjini Abuja, wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wamewaenzi wenzao waliouawa shahidi walipovamia na wanajeshi wa Nigeria mnamo Julai 25 mwaka 2014.

Katika tukio hilo la kutisha, wanachama 35 wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria waliuawa shahidi kwa kufyatuliwa risasi na askari wa Nigeria.

Katika taarifa, jeshi la Nigeria lilidai kuwa lililazimika kuchukua hatua hiyo kwa ajili ya kujilinda, madai ambayo yalitupiliwa mbali na viongozi wa harakati hiyo ya Kiislamu.

Miamala mibaya ya wanajeshi wa Nigeria mkabala wa Waislamu wa Kishia

Miezi michache baadaye, jeshi la Nigeria lilitekeleza ukatili mwingine jimboni Zaria mwaka 2015, ambapo wanachama wengine 340 waliuawa kinyama.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2015 jeshi la Nigeria lilivamia shughuli za kidini katika Husseiniya ya Baqiyatullah katika mji wa Zaria na kuua karibu wafuasi elfu mbili wa Sheikh Zakaky waliokuwa wamekusanyika katika eneo hilo la ibada, mbali na kumtia nguvuni kiongozi huyo wa Kiislamu na mkewe ambao wanazuiliwa hadi hii leo. 

 

 

Tags