Jul 26, 2021 12:28 UTC
  • Corona Tanzania; Marufuku kuingia kwenye usafiri wa umma bila barakoa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Amos Makalla amewataka Wananchi kuchukuwa tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Corona ambapo amepiga marufuku wananchi kuingia kwenye vyombo vya usafiri na sehemu za kutoa huduma bila kuvaa barakoa.

Makalla ametoa maelekezo hayo kufuatia muongozo uliotolewa na Wizara ya Afya ambapo amesema watafanya ziara za kushtukiza kwenye vituo vya daladala, feri, stendi, mabasi ya mwendokasi, maeneo ya masoko na sehemu zote za kutoa huduma ili kuangalia utekelezaji wa agizo hilo.

Aidha Makalla amesema serikali imejipanga kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa wote watakaofika hospitalini na kuwataka wananchi watakaoona dalili za Corona kuwahi vituo vya afya.

Wizara ya Afya nchini Tanzania hivi karibuni ilitangaza masharti mapya yanayolenga kusaidia kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo.

Abiria aliovaa barakoa katika usafiri wa umma Tanzania

Watu nchini humo wametakiwa kuvaa barakoa kila wakati na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, ikiwa ni pamoja na wito wa kuahirishwa kwa sherehe za harusi, huku mikusanyiko ya watu kwenye majumba ya ibada ikitakiwa kupungua.

Haya yanajiri siku chache baada ya Waziri wa Afya wa Tanzania, Dk Dorothy Gwajima kusema hadi sasa jumla ya watu 29 wamefariki dunia kutokana na wimbi la tatu la Covid-19 nchini humo.

Tags