Jul 27, 2021 02:32 UTC
  • Algeria yalaani Israel kuteuliwa mwanachama mtazamaji wa Umoja wa Afrika

Algeria imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel kibali cha kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Algeria sambamba na kulaani vikali uamuzi huo imesema kuwa, hatua hiyo haikubaliki.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa pasi na kuweko mashauriano ya hapo kabla baina ya nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika.

 Alkhamisi iliyopita, utawala haramu wa Israel ulitangaza kuwa umeidhinishwa kuwa mwanachama mtazamaji wa AU baada ya eti jitihada za kidiplomasia za karibu miongo miwili.

Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita, Shirikisho la Wanahabari wa Afrika (FAJ) liliutaka Umoja wa Afrika (AU) ulaani mienendo ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwashambulia wanahabari wa Palestina, sanjari na kuubebesha dhima kisheria utawala huo kwa jinai zake dhidi ya wanahabari hao kila leo.

 

Kabla ya Algeria, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) pia imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel kibali cha kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo.

HAMAS ilisema katika taarifa yake kwamba, uamuzi huo wa Umoja wa Afrika si tu utaupa uhalali utawala ghasibu wa Israel wa kuendelea kupora ardhi zaidi za Wapalestina, lakini pia utaushajiisha na kuupa nguvu utawala huo haramu za kuendelea na njama yake ya kutaka kufuta haki za Wapalestina.

Tags