Jul 27, 2021 07:47 UTC
  • Wanachuo waandamana Kongo kupinga kuuliwa mwenzao kwa kutovaa barakoa

Wanafunzi wa Chuo Kikuu mjini Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameendelea kuandamana kulalamikia kitendo cha polisi cha kumuua mwanachuo mwenzao kwa madai ya kutovaa barakoa ya kujikinga na maambukizi ya corona.

Polisi ya Kongo wanadaiwa mara kwa mara kuwabughudhi wananchi na kupokea pesa kama tozo ya fidia ya kutovaa barakoa hadharani. 

Maandamano ya wanafunzi  wa Chuo Kikuu huko Kinshasa yaliibuka baada ya polisi mmoja kumpiga risasi mwenzao mwishoni mwa wiki kwa kutovaa barakoa wakati akirekodi filamu katika mitaa ya mji mkuu Kinshasa. Wanachuo wenzake wa mwanafunzi aliyeuawa na polisi kwa kupigwa risasi kwa jina la Honore Shama wameshindwa kuzuia hasira na ghadhabu zao.

Baadhi yao wamesika wakisema kuwa wameshtushwa na mauaji ya mwanachuo mwenzao ambaye ameuawa kwa sababu tu ya barakoa ambayo thamani yake haifiki hata faranga 100. Mwanafunzi mwingine aliyeshuhudia makabiliano na polisi na mwendazake huyo amesema kuwa, polisi alimwamuru mwenzake kuvaa barakoa lakini licha ya maelezo yaliyotolewa na mhanga na baada ya kumuonyesha polisi barakoa yake huku akisubiri kupewa pesa kama ilivyozoeleka alipandwa na hasira na kumtuhumu mwanafunzi huyo kuwa anapingana na amri yake na kisha akamfyatulia risasi. Mwanafunzi aliyeuliwa na polisi alikuwa akirekodi filamu katika fremu ya mafunzo yake ya vitendo. 

Jenerali Sylvano Kasongo Mkuu wa Polisi ya Kinshasa amesema kuwa, polisi aliyehusika na mauaji amekimbia na msako unaendelea. Ni wajibu kuvaa barakoa (mask) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kukabiliana na maambukizi ya corona.

Kuvaa barakoa Kongo DR ni wajibu

 

Tags