Jul 27, 2021 15:27 UTC
  • Mamia ya raia wauawa katika eneo la Somali nchini Ethiopia

Serikali ya jimbo la Somali huko mashariki mwa Ethiopia imewatuhumu waasi kutoka jimbo jirani la Afar kuwa wameua mamia ya raia katika shambulio la hivi karibuni.

Msemaji wa serikali ya jimbo la Somali, Ali Bedel ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wanamgambo kutoka eneo la Afar siku ya Jumamosi walishambulia maeneo ya Gedamaytu na Gabraiisa katika jimbo la Somali na kuua mamia ya raia.

Kadhalika maafisa wengine wawili wa serikali ya jimbo la Somali wamethibitisha kutokea mauaji hayo ya ummati, ingawaje hawajaeleza idadi ya wahanga wa shambulio hilo la mwishoni wa wiki.

Habari zaidi zinasema kuwa, timu ya madaktari imetumwa katika maeneo hayo yaliyoshambuliwa jimboni Somali, ili kutoa matibabu kwa idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa.

Wanajeshi wa Ethiopia katika operesheni ya kiusalama eneo la Tigray la kaskazini mwa nchi

Ahmed Koloyta, msemaji wa jimbo la Afar amekwepa kulizungumzia shambulio hilo alipotakiwa kufanya hivyo na shirika la habari la Reuters.

Kabla ya hapo, Jenerali Tsadkan Gebretensae, afisa wa ngazi ya juu wa Harakati ya Ukombozi ya eneo la Tigray (TPLF) alisema wapiganaji wa kundi hilo wamepata mafanikio makubwa katika makabiliano baina yao na wapiganaji waitifaki wa serikali kuu ya Addis Ababa katika barabara ya mji wa Chercher kuelekea Mille eneo la Afar, na sasa hawana kitu kinachowazuia kelekea katika mji mkuu wa nchi.

Tags