Jul 28, 2021 11:14 UTC
  • Spika wa Zimbabwe: Marekani, muasisi wa ukiukaji wa haki za binadamu

Spika wa Bunge la Kitaifa la Zimbabwe ameitaja Marekani kama muasisi, chimbuko na taifa linaloongoza kwa ukiukaji wa haki za binadamu duniani.

Jacob Francis Mudenda, Spika wa Bunge la Zimbabwe amesema hayo katika mazungumzo yake na Abbas Navazani, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa serikali ya Zimbabwe amesisitiza kuwa, Marekani ndiyo nchi inayoongoza kwa kukanyaga haki za binadamu duniani, hususan haki za watu weusi (wenye asili ya Afrika).

Kadhalika ameashiria shambulio dhidi ya Kongresi ya Marekani na kubainisha kuwa, kitendo hicho ni mfano wa wazi wa namna siasa za nchi hiyo ya kibeberu ni za kimwanagenzi.

Aidha Spika wa Bunge la Zimbabwe na Abbas Navazani, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika wamekosoa vikali vikwazo vilivyo kinyume cha sheria vya Marekani dhidi ya Tehran na Harare.

Ugaidi wa kiuchumi wa US

Wawili hao vile vile wamesisitizia haja ya kuimarishwa ushirikiano katika taasisi za kimataifa, kukabiliana na maamuzi ya upande mmoja ya Marekani na kupigwa jeki jitihada za kupambana na sera ya ugaidi wa kiuchumi ya Washington.

Wakati huo huo, maafisa hao wawili wa Iran na Zimbabwe wametoa mwito wa kupanuliwa uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbali mbali kama vile kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia, huku wakisisitiza kuwa diplomasia ya kibunge baina ya Tehran na Harare inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa kidugu baina ya mataifa haya mawili.

 

Tags