Jul 28, 2021 11:16 UTC
  • Mripuko wa kipindupindu waua watu 479 nchini Nigeria

Mamia ya watu wameripotiwa kuaga dunia kutokana na mripuko wa maradhi ya kipindupindu nchini Nigeria.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria (NCDC) imesema kwamba, kesi za ugonjwa huo zilizorekodiwa kufikia sasa ni 19,000, vikiwemo vifo 479.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, tangu mripuko huo uliporitiwa kwa mara ya kwanza mwezi Januari mwaka huu hadi sasa, ugonjwa huo umeshaenea katika majimbo 15 ya nchi hiyo, ukiwemo mji mkuu Abuja. 

Ugonjwa wa kipindupindu husababishwa na bakteria aina ya Vibrio Cholera na huenezwa kwa kunywa maji yasiyo salama. Dalili za ugonjwa huo ni maumivu ya tumbo, kuharisha, kutapika pamoja na homa.

Mrundiko wa wagonjwa wa kipindupindu hospitalini Nigeria

Miripuko ya maradhi hayo hatarishi huripotiwa nchini Nigeria mara kwa mara, hususan katika misimu ya mvua za masika zinazoambatana na mafuriko.

Takwimu zinaonesha kuwa, watu bilioni 1.4 wapo katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu kote duniani, ambapo kwa wastani kesi milioni 2.8 za maradhi hayo huripotiwa kila mwaka, mbali na vifo zaidi ya 91,000.

 

Tags