Jul 28, 2021 13:50 UTC
  • Rais Samia Suluhu Hassan akipewa chanjo ya corona
    Rais Samia Suluhu Hassan akipewa chanjo ya corona

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania leo ameongoza zoezi la uzinduzi wa kutoa chanjo ya corona nchini humo akisema asingekuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa kuchanjwa chanjo hiyo kama isingekuwa salama.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatano katika uzinduzi wa kutoa chanjo hiyo, kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Rais jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo inakuja baada ya Tanzania kupokea zaidi ya dozi milioni 1.05 za chanjo aina ya Johnson & Johnson wiki iliyopita zilizotolewa kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa kutoa chanjo kwa nchi mbalimbali, Covax.

Hatua hiyo ya Rais wa Tanzania imewatoa hofu baadhi ya wananchi wakiwemo wanasiasa na wabunge wanaotilia shaka usalama wa chanjo zinazotolewa kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya corona.

“Nategemewa kama mama, kama bibi, kama Rais, kama Amiri Jeshi Mkuu, nisingejitoa mwenyewe nikajipeleka kwenye kifo, nikajipeleka kwenye hatari nikijua kwamba nina majukumu yote haya yananitegemea", amesema Rais wa Tanzania akisisitiza usalama wa chanjo hiyo ya kupambana na virusi vya corona.

Ameongeza kuwa amekubali kwa hiari yake kuchanja akijua kwamba ndani ya mwili wake ana chanjo kadhaa ambazo ameishi nazo kwa miaka 61 sasa kwani tangu amezaliwa kuna chanjo mbalimbali wamekuwa wakichanjwa, mbali na zingine wanazochanjwa njiani wakiwa wanasafiri ikiwemo ya homa ya manjano.

“Kwa wale ambao koo zao hazijaguswa, hawajapata madhara ya maradhi haya wanaweza kusema wanavyotaka. Lakini nenda leo Moshi, nenda Arusha ,nenda Kagera, hata Dar es Salaam uonane na zile koo ambazo zimeshaguswa na haya maradhi wana maneno ya kukuambia, na kama wangeweza leo wote wangekuwa hapa kutaka kuchanja kuepukana na ile hasara walioipata", amesisitiza Rais Samia Suluhu Hassan.

Hatua hiyo ya Rais Samia imefuatiwa na viongozi wengine wa ngazi za juu wa Tanzania katika uzinduzi wa kampeni ya kutoa chanjo ya corona kwa Watanzania mbao pia wamejitokeza kupokea chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 akiwemo Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma, Waziri wa Afya Dorothy Gwajima, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro na viongozi wa dini. 

Rais wa Tanzania amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi ili kupata chanjo.
Hata hivyo Rais Samia Suluhu amesema chanjo iliyopo hivi sasa nchini humo ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya Watanzania.

Tags