Jul 29, 2021 02:33 UTC
  • Afrika Kusini yapinga Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika AU

Serikali ya Afrika Kusini imepinga kitendo cha kutambuliwa utawala haramu wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika (AU.

Serikali ya Afrika Kusini imesema kuwa uamuzi huo si wa kiadilifu na wala hauwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile.

Hatua hiyo ya Afrika Kusini inafuatia uamuzi wa Algeria ambayo pia imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel kibali cha kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Algeria sambamba na kulaani vikali uamuzi huo imesema kuwa, hatua hiyo haikubaliki.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa pasi na kuweko mashauriano ya hapo kabla baina ya nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika.

Vilevile wanaharakati kutoka nchi tano za kaskazini mwa Afrika ambazo ni Algeria, Tunisia, Morocco, Libya na Mauritania wamesisitiza udharura wa kukabiliana na hatua ya baadhi ya nchi ya kuanzisha uhusiano rasmi wa na utawala ghasibu wa Israel.

Mwezi uliopita pia Shirikisho la Wanahabari wa Afrika (FAJ) liliutaka Umoja wa Afrika (AU) ulaani mienendo ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwashambulia wanahabari wa Palestina, sanjari na kuubebesha dhima kisheria utawala huo kwa jinai zake dhidi ya wanahabari hao kila leo.

Kabla ya Algeria, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) pia imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel kibali cha kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo. 

 Alkhamisi iliyopita, utawala haramu wa Israel ulitangaza kuwa umeidhinishwa kuwa mwanachama mtazamaji wa AU baada ya eti jitihada za kidiplomasia za karibu miongo miwili.

Tags