Jul 29, 2021 02:56 UTC
  • Hukumu ya kuachiwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe yatolewa

Ofisi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria jana usiku iliripoti taarifa ya kutolewa hukumu ya kuachiwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe.

Shirika la habari la Farsi limeripoti kuwa, ofisi ya Sheikh Zakzaky imetangaza kuwa mahakama katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria imewafutia tuhuma zote zilizokuwa zikiwakabili Sheikh Zakzaky na mkewe na kuamuru kuachiwa huru. Ofisi hiyo imeongeza kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe wataachiwa huru karibuni. Hukumu hiyo inatajwa kama ushindi kwa kambi ya muqawama mkabala wa ukandamizaji na dhulma kubwa ya serikali ya Nigeria.  

Serikali ya Nigeria hadi kufikia sasa ilikuwa imezuia kuachiwa huru mwanazuoni huyo mtajika wa Nigeria na mkewe kwa visingizio mbalimbali na hata kuwanyima ruhusa ya kwenda kupatiwa matibabu. 

Katika miezi ya karibuni ambapo hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky ilizidi kudhoofu taasisi mbalimbali za kutetea haki za binadamu zilitoa mwito mara kadhaa zikitaka kuachiwa huru Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. 

Sheikh Ibrahim Zakzaky 

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walitiwa mbaroni Disemba 13 mwaka 2015 wakati jeshi la Nigeria liliposhambulia Husseiniya ya Baqiyatullah katika mji wa Zaria nchini humo. Siku hiyo jeshi la Nigeria liliufyatulia risasi waumini waliokuwa wanashiriki marasimu ya kidini katika husseiniya hiyo katika nyumba ya mwanazuoni huyo na kuwauwa mamia ya watu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky.