Jul 29, 2021 11:04 UTC
  • Massoud Shajareh
    Massoud Shajareh

Mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu wa Kiislamu amesema kufutiwa tuhuma zote kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe baada ya mashaka makubwa ya miaka sita, ni kielelezo cha kufeli sera za Abuja za kuwanyanyasa na kuwakandamiza wanaharakati hao.

Massoud Shajareh ambaye ni mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kiislam huko London, ameyasema hayo katika mahojiano yake na Press TV na kuongeza kuwa, serikali ya Nigeria imeshindwa kuthibitisha kesi yoyote inayomkabili Sheikh Zakzaky kama ilivyokuwa huko nyuma. 

Shajareh amesema inashangaza kuona jinsi kampeni hii ya manyanyaso na ukandamizaji ilivyochukua muda mrefu licha ya kwamba Mahakama Kuu ya Nigeria mwaka 2016 iliamuru kuachiliwa Sheikh Zakzaky na mkewe. 

Mwanaharakati huyo wa kutetea haki za binadamu amesisitiza kwamba mienendo ya serikali ya Nigeria dhidi ya Sheikh Zakzaky na wafuasi wake "itabaki kama alama nyeusi na mbaya kwa Nigeria," akibainisha kuwa, "Serikali ya Abuja haiwezi kuendelea kutenda hivyo kwa raia wake."

Sheikh Zakzaky

Itakumbukwa kuwa mahakama ya jimbo la Kaduna nchini Nigeria imefutia tuhuma zote zilizokuwa zikiwakabili Sheikh Zakzaky na mkewe na kuamuru waachiwe huru. Ofisi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky imetangaza kuwa, kiongozi huyo na mkewe wataachiwa huru karibuni. Hukumu hiyo inatajwa kama ushindi kwa kambi ya muqawama mkabala wa ukandamizaji na dhulma kubwa ya serikali ya Nigeria.  

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walitiwa mbaroni Disemba 13 mwaka 2015 wakati jeshi la Nigeria liliposhambulia kituo cha kidini cha Baqiyatullah katika mji wa Zaria. Siku hiyo jeshi la Nigeria liliwafyatulia risasi waumini waliokuwa wakishiriki shughuli ya kidini katika eneo hilo na kuwauwa mamia ya watu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky. 

Tags