Jul 30, 2021 02:20 UTC
  • Amir wa Qatar amtaka Rais wa Tunisia kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kupitia mazungumzo na vyama vya siasa

Amir wa Qatar amempendekezea Rais wa Tunisia kufanya mazungumzo na vyama vya siasa ili kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Tamim bin Hamad al-Thani ametoa pendekezo hilo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Rais Kais Saied wa Tunisia ambapo amesisitiza pia udharura wa kuheshimiwa katiba ya nchi.

Amir wa Qatar amesema katika mazungumzo hayo kwamba, kuna ulazima wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuivusha Tunisia katika kipindi hiki cha mgogoro. Aidha amesema kuna umuhimu wa kufanyika mazungumzo baina ya serikali na vyama vya siasa vya nchi hiyo ili kutafuta njia mwafaka za kuuupatia ufumbuzi mgogoro huo.

Maandamano ya wananchi wa Tunisia

 

Baada ya kusimamisha Bunge na kumtimua Waziri Mkuu Hichem Mechichi Jumapili iliyopita, na vilevile kuwafukuza mawaziri wa ulinzi na sheria siku moja baadaye, Rais Saied ameamuru kufutwa kazi maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa serikali ya Tunis.

Rais huyo wa Tunisia mwenye umri wa miaka 63, mhadhiri wa zamani wa sheria na mwanagenzi wa kisiasa ambaye alishinda kwa kishindo uchaguzi wa urais wa 2019, ametoa amri ya kufukuzwa orodha ndefu ya maafisa wakuu wa serikali, pamoja na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Jeshi. Juzi pia alimtimua Mkurugenzi Mtendaji wa runinga ya taifa ya al Wataniya. Maamuzi hayo ya Rais Kais Saied wa Tunisia yamepingwa vikali na vyama vya upinzani na wanaharakati wa masuala ya siasa.