Jul 30, 2021 02:20 UTC
  • Kamanda mwandamizi wa kundi la al-Shabab ajisalimisha kwa vikosi vya serikali ya Somalia

Abdirazak Abdullahi Mohamed, kamanda mwandamizi wa kundi la kigaidi la al-Shabab amejisalimisha kwa vikosi vya serikali vya Somalia.

Hayo yamelezwa na Mohamed Jama, kamanda wa Jeshi la Taifa la Somalia katika mji wa Garbaharey ambaye amebainisha kwamba, kamanda huyo wa wanamgambo wa al-Shabab amejisalimisha kwa vikosi vya serikali katika mji huo ulioko kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Afisa huyo wa jeshi la Somalia amesema kuwa, kamanda huyo wa wanamgambo wa al-Shabab amekuwa mwanachama wa kundi hilo la kigaidi kwa miaka sita na kwamba, alihusika katika operesheni nyingi za al-Shabab katika miji ya Gedo na Bay.

Akizungumza na waandishi wa habari, Abdirazak Abdullahi Mohamed amesema kuwa, ameamua kuachana na uasi kwa hiari yake na kujiunga na vikosi vya serikali ya Somalia.

Kundi la kigaidi la al-Shabab limehusika na milipuko mingi ya mabomu nchini Somalia ambayo imepelekea maelfu ya watu kuuawa

 

Hayo yanajiri siku chache tu, baada ya Jeshi la Taifa la Somalia kutangaza kwamba, limemtia mbaroni Ali Mohamed Adan, kamanda mkuu wa operesheni za kigaidi za kundi hilo katika jimbo la Lower Shabelle.

Maafisa wa Jeshi la Taifa la Somalia wamesema kwamba, Adan ndiye mhusika mkuu wa aghalabu ya mashambulizi yaliyofanyika katika eneo hilo, zikiwemo hujuma za mabomu ya kutegwa kando kando ya barabara kuu za jimbo hilo.

Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.