Jul 30, 2021 03:37 UTC
  • Waislamu katika miji ya Nigeria washerehekea kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe

Duru za habari zimeripoti kuwa, furaha, vifijo na sherehe zimeshamiri katika baadhi ya miji ya Nigeria kufuatia kutangazwa habari ya kuachiwa huru kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mke wake.

Televisheni ya Al-Alam imetangaza kuwa, wananchi Waislamu katika majimbo na miji ya Zaria, Kano, Bauchi, Katsina, Gombi na Borno huko kaskazini mwa nchi, walimiminika kwenye mitaa na barabara za miji hiyo kusherehekea kuachiwa huru Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe, ambao waliwekwa gerezani kwa muda wa takriban miaka sita pasi na kupatikana na hatia ya kosa lolote.

Siku ya Jumatano, Sheikh Zakzaky na mke wake waliachiwa huru baada ya kuwekwa jela kwa muda wa miaka sita katika hali na mazingira ya kikatili na kinyama.

Kwa mujibu wa duru za habari, baada ya vyombo vya dola kumshikilia kiongozi huyo wa kidini kwa muda wote huo, hatimaye mahakama ya nchi hiyo imemtoa hatiani Sheikh Zakzaky na mkewe kuhusiana na mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake walikamatwa Desemba 13, 2015 katika hujuma na shambulio lililofanywa na askari wa jeshi la serikali dhidi ya Husainiya iliyoko katika mji wa Zaria.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na Mke wake

Siku hiyo aliyokamatwa Sheikh Zakzaky, vikosi vya jeshi la Nigeria viliwafyatulia risasi Waislamu waliokuwa wamekusanyika kwenye Husaniya hiyo na nyumba yake na kuwaua shahidi mamia kadhaa miongoni mwao, wakiwemo wana watatu wa kiume wa kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo. 

Wakili wa Sheikh Zakzaky alitangaza hivi karibuni kuwa utawala wa Saudi Arabia umewapa viongozi wa Nigeria mamilioni ya dola ili wamuue mwanazuoni huyo wa Kiislamu.

Katika miezi ya karibuni, wananchi wa Nigeria walifanya maandamano ya amani mara kadhaa katika miji mbalimbali kutaka Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiwe huru, lakini vyombo vya usalama vya utawala wa Abuja vilitumia mkono wa chuma kuzima na kukandamiza maandamano hayo.../