Jul 30, 2021 07:17 UTC
  • Mahakama ya Misri yatoa hukumu ya kifo kwa wanachama wengine 24 wa Ikhwanul Muslimin

Mahakama ya Misri imetoa hukumu ya kifo kwa wapinzani 24 wa mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa dhidi ya rais halali wa zamani wa nchi hiyo marehemu Muhammad Morsi.

Watu hao ambao hawakutajwa majina yao, wamehukumiwa kifo kwa tuhuma za kuandamana katika mkoa wa al Bahira kaskazini mwa nchi hiyo kulalamikia mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa na waziri wa ulinzi wakati huo Abdel Fattah Al Sisi dhidi ya rais wa zamani Muhammad Morsi.

Hukumu hiyo ilitolewa hapo jana, wakati mnamo tarehe 14 Juni mahakama ya rufaa ya Misri iliidhinisha kutekelezwa hukumu ya kifo kwa viongozi 12 wa harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin.

Watu hao walitiwa hatiani kwa kosa la kuandaa mgomo wa kuketi katika uwanja wa mzunguko wa Raabiatul-Adawiyah mwaka 2013 na mikusanyiko ya umma ya kumuunga mkono Morsi.

Viongozi waandamizi wa Ikhwanul Muslimin, wakiwemo waliofia magereani kwa mateso na waliohukumiwa vifungo vya maisha jela

Katika miaka ya karibuni, vyombo vya mahakama vya Misri vilivyo chini ya serikali ya rais Abdel Fattah Al Sisi vimetoa hukumu za vifo au vifungo vya muda mrefu jela kwa wanachama wengi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin kwa tuhuma mbali mbali bandia na zisizo na msingi.

Al Sisi aliongoza mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013 yaliyomuondoa madarakani rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri hayati Muhammad Morsi.

Tangu alipoingia madarakani mwaka 2014 na kwa kutumia kichaka cha uungaji mkono wa madola ya Magharibi, Abdel Fattah Al Sisi amekuwa akitekeleza sera za ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa utawala wake.

Katika miezi ya karibuni, asasi nyingi za kimataifa na za kutetea haki za binadamu zimekuwa zikitoa indhari kuhusu utendaji wa kiongozi huyo katika masuala ya uhuru wa kijamii na kisiasa na ukiukaji wa haki za binadamu.../

Tags