Jul 30, 2021 08:02 UTC
  • Mwanajudo wa Algeria: Nimefurahi kuona hatua yangu imeikasirisha Israel

Fath-i Nurin, mwanamichezo wa mchezo wa Judo wa Algeria ambaye kwa sababu ya kutokubali kuutambua utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kwa ajili kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina hakuwa tayari kupambana na mshindani kutoka utawala huo katika mashindano ya Olimpiki ya Tokyo 2020, amesema, amefurahia hatua yake hiyo kwa kuwa imeikasirisha Tel Aviv.

Alipowasili uwanja wa ndege wa Algiers Jumatano usiku, na ijapokuwa alirudi nyumbani bila kuiletea nchi yake medali yoyote, Nurin alilakiwa kwa shangwe na furaha kubwa kuwahi kushuhudiwa na wananchi wa Algeria kutokana na msimamo wake wa kuunga mkono malengo matukufu ya wananchi wa Palestina.

Akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege, mwanajudo huyo wa Algeria katika mashindano ya Olimpiki ya Tokyo alisema, alichukua uamuzi huo wa kukataa kupambana na mwanamichezo Mzayuni kwa mashauriano na kocha wake.

Ameongezea kusema: "uamuzi niliochukua, kwanza ni wa kujivunia mimi mwenyewe na kisha ni hatua ya fahari na kujivunia kwa wananchi na serikali ya Algeria, kwa sababu Rais wa nchi yetu Abdelmadjid Tebboune naye pia ameitangazia dunia nzima kwamba, sisi hatuoni kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel kuwa ni tukio la kheri na tunaunga mkono malengo matukufu ya watu wa Palestina."

Fath-i Nurin

Fat-hi Nurin amesisitiza kwa kusema: "Nimefurahi kuona utawala wa Kizayuni umekasirika na kutokana na kutumiwa jumbe za kuungwa mkono katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu."

Mwanajudo huyo wa Algeria aidha amesema, alishtuka alipoona katika kura ameangukia kupambana na mwanamichezo wa utawala wa Kizayuni kwa sababu hakutarajia jambo hilo, lakini hakuwa na shaka hata chembe katika uamuzi aliochukua wa kukataa kupambana na mshindani wake huyo Muisraeli.

Gazeti la Kiebrania la Yediot Ahronot liliandika katika toleo lake la hivi karibuni kuwa, historia imethibitisha kuwa ukweli hauwezi kubadilishwa na kwamba mapatano ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu yako makaratasini tu, lakini katika mazingira halisi ya mahusiano ya kiutu, wanamichezo wa nchi za Kiarabu wamethibitisha kuwa, kwa mtazamo wao, hakuna nchi inayoitwa Israel.../

Tags