Jul 30, 2021 08:05 UTC
  • Rais wa Tunisia awafutia rasmi Wabunge kinga za kisheria za kutoshtakiwa

Rais Kais Saied wa Tunisia amefuta rasmi kinga ya kisheria waliyokuwa nayo wabunge wote wa bunge la nchi hiyo.

Duru za habari za Tunisia zimetangaza alifajiri ya kuamkia leo kuwa, Rais Kais Saied alitoa dikrii usiku wa kuamkia leo ya kubatilisha rasmi kinga ya kutoshtakiwa waliyonayo wabunge wote, ambayo itatekelezwa katika kipindi chote cha kusitishwa shughuli za chombo hicho kikuu cha utungaji sheria.

Katika taarifa aliyotoa usiku wa kuamkia leo, Saied amesisitiza kuwa hatua zote za dharura alizochukua hadi sasa zinaendana na katiba ya nchi, na hakuna yoyote inayokiuka haki na uhuru.

Katika taarifa yake hiyo, Rais wa Tunisia amesema: "Ninakuelezeni nyinyi na dunia nzima kwamba, nimedhamiria kwa dhati kutekeleza maandiko ya katiba; na nina shauku kubwa zaidi kuliko wao kulinda haki na uhuru wa raia; na sheria zimetekelezwa kikamilifu."

Bunge la Tunisia

Siku ya Jumapili iliyopita Rais Kais Saied alichukua hatua ya kushtukiza ya kumfuta kazi Spika wa Bunge na Waziri Mkuu wa nchi hiyo na kudhibiti madaraka yote ya nchi.

Wapinzani wake wameitafsiri hatua hiyo kuwa ni mapinduzi baridi aliyofanya kwa kushirikiana na jeshi la nchi hiyo. 

Spika wa Bunge la Tunisia, Rached Ghannouchi amesema hatua aliyochukua Rais Kais Saied ni mapinduzi dhidi ya mapinduzi ya wananchi, katiba ya nchi na uhuru wa taifa.

Hadi sasa miito mbalimbali imetolewa na ingali inaendelea kutolewa kimataifa kutaka mgogoro na taharuki hiyo ya kisiasa iliyotokea Tunisia itatuliwe kwa njia ya mazungumzo.../