Jul 30, 2021 12:41 UTC
  • ICC yabatilisha waranti wa kukamatwa mke wa aliyekuwa rais wa Kodivaa

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetupilia mbali waranti wa kukamatwa Simone Gbagbo, mke wa Laurent Gbagbo, rais wa zamani wa Ivory Coast.

Hukumu ya ukurasa saba ya mahakama hiyo ya mjini Hague nchini Uholanzi iliyoanikwa paruwanja jana Alkhamisi inaonesha kuwa, waranti wa kutiwa mbaroni Simone Gbagbo ambaye alikuwa anaandamwa na mashitaka ya jinai dhidi ya kibadamu kama vile mauaji, ubakaji, mateso na ukandamizaji, kufuatia hatua ya mumewe kukataa kukabidhi madaraka kwa Alassane Ouattara, aliyeshinda uchaguzi wa 2010.umetenguliwa.

Ange Rodrigue Dadje, wakili wa Simone Gbagbo amesema, "habari njema kwa Simone Gbagbo, sasa yuko huru kutembea pahala popote duniani." 

Laurent Gbagbo, aliyekuwa rais wa Ivory Coast alirejea nyumbani mwezi uliopita wa Juni baada ya kushinda kesi muhimu iliyokuwa ikimkabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Rais Alassane Outtara (kulia) alikutana na mtangulizai wake Gbagbo hivi karibuni na kuzika uhasama wao wa kisiasa wa muda mrefu

Gbagbo mwenye umri wa miaka 76, ambaye alichaguliwa kuwa rais wa Ivory Coast mwaka 2000 alikataa kuyakubali matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010 yaliyoonyesha kuwa alishindwa na mshindani wake mkuu Alassane Ouattara.

Zaidi ya watu elfu tatu waliuawa katika mapigano ya miezi kadhaa yaliyohusisha pande tiifu kwa wanasiasa hao, kabla ya Gbagbo kutiwa nguvuni Aprili 2011 na kukabidhiwa kwa mahakama ya ICC na kufunguliwa kesi ya kuhusika na jinai ya dhidi ya binadamu, ambayo hatimaye alishinda baada ya kutopatikana na hatia mwezi Machi mwaka huu.

Tags