Jul 31, 2021 03:18 UTC
  • Wachezaji watano wa soka wauawa katika shambulizi la kigaidi Kismayo

Wachezaji wasiopungua watano wa soka wameuawa katika mlipuko wa bomu kwenye basi lililokuwa limebeba timu ya mpira wa miguu katika mji wa Kismayo huko kusini mwa Somalia.

Afisa mmoja wa polisi ya Somalia amesema bomu lililokuwa limetegwa kwenye basi la timu ya mpira wa miguu ya JCCI lililipuka muda mfupi baada ya basi kung'oa nanga likielea uwanjani kwa ajili ya mechi ya ufunguzi wa mashindano ya kanda ya Jubaland.

Kapteni Ahmed Farah amesema kuwa, wachezaji 5 wamethibitika kuuawa na wengine zaidi ya 12 wamejeruhiwa. Amesema wachezaji wengine kadhaa hawajulikani waliko.

Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo.

Basi la timu ya mpira wa miguu ya JCCI likitekelea kwa moto

Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo wa Somalia ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulizi hilo na kulituhumu kundi la al Shabab lenye mfungamano la al Qaida kuwa ndilo lililohusika na hujuma hiyo.

Somalia imekuwa kwenye vita kali dhidi ya kundi la kigaidi la al Shabab lililoanzishwa mwaka 2004 na kutekeleza mashambulizi mengi ya kigaidi ndani na nje ya nchi hiyo.