Jul 31, 2021 13:41 UTC
  • UNICEF: Zaidi ya watoto 100,000 wa Tigray Ethiopia hatarini kupoteza maisha kwa utapiamlo

Zaidi ya watoto 100,000 katika jimbo la Tigray la Ethiopia, eneo la mapigano, wako katika hatari ya lishe inayohatarisha maisha katika miezi 12 ijayo.

Hayo yameelezwa na msemaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ambaye amebainisha kwamba, hali ya watoto katika jimbo hilo ni mbaya.

Marixie Mercado, akirudi kutoka Tigray, amebaini kwamba mmoja kati ya wanawake wawili wajawazito au wanaonyonyesha wanakabiliwa na utapiamlo mkali, na kuwafanya wao na watoto wao kuathirika zaidi na magonjwa.

"Hofu yetu mbaya juu ya afya ya watoto katika jimbo la Tigray lenye migogoro kaskazini mwa Ethiopia imethibitishwa," amesema katika mkutano wa Umoja wa Mataifa huko Geneva. Ameongeza kuwa hakukuwa na makadirio ya vifo na ametoa wito kwa nchi mbali mbali kutoa misaada ya kibinadamu bila kizuizi na misaada hiyo iweze kuwafikia walengwa katika eneo hilo.

Wakimbizi katika jimbo la Tigray

 

Wakati huo huo, Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR ) amesema kuwa ana wasiwasi mkubwa juu ya hali ya wakimbizi wa Eritrea katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana, kwa madai kuwa wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi. Hadi sasa mapigano hayo yamewalazimisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbzi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na ukosefu wa chakula.